Followers

Sunday, January 4, 2009

Serikali na barabara za Tanzania

Barabara Kuu

Mtandao wa Barabara Kuu upo katika mfumo wa Kanda Kuu za usafirishaji. Utaratibu huu una lengo la kuhakikisha kwamba, barabara zote za kila kanda zinapitika na kutoa mtiririko wa usafiri wenye uhakika kati ya kanda moja na nyingine na kuiwezesha Tanzania kutumia kwa ukamilifu faida ya Kijiografia iliyonayo katika kuziunganisha nchi kadhaa tunazopakana nazo na bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Mbambabay, Kigoma, Bukoba na Mtwara. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mtandao wa Barabara Kuu umeimarika na kuwa na jumla ya kilometa 10,601. Kati ya hizo, kilometa 5,002 ni za lami na kilometa 5,599 ni za changarawe ikilinganishwa na mwaka 2005 ambapo tulikuwa na Barabara Kuu zenye urefu wa kilometa 9,934.4, na kati ya hizo, kilometa 3,913.8 zilikuwa za lami na kilometa 6,020.6 za changarawe.

Aidha miradi 12 kati ya 17 iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya tatu imekamilika na iliyobaki 5 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Miradi iliyokamilika ni pamoja na Singida – Shelui, Nzega – Ilula na Tinde - Isaka, Nangurukuru – Mbwemkuru, Mbwemkuru – Mingoyo, Mkuranga – Kibiti, Pugu – Kisarawe, Geita – Buzirayombo, Buzirayombo – Kyamiorwa , Singida – Manyoni (sehemu ya Singida – Isuna), Dodoma – Morogoro, Tarakea – Rongai – Kamwanga na Barabara ya Sam Nujoma (Dar es Salaam).

Miradi 5 ambayo ujenzi wake unaendelea ni Daraja la Umoja, Dodoma – Manyoni, Tarakea – Kamwanga, Kagoma – Biharamulo – Lusahunga, na Marangu - Rombo Mkuu – Tarakea.

Aidha Serikali ya Awamu Nne imeanzisha miradi ya Daraja la Ruvu (Umekamilika), Mbeya – Chunya – Makongolosi sehemu ya Mbeya – Lwanjiro (km 36), Masasi – Mangaka (km 54), Arusha – Namanga (km 105), barabara ya Kilwa (awamu ya kwanza km 5 imekamilika na awamu ya pili km 5.6 inaendelea), Nelson Mandela DSM (km 15.6), Manyoni – Isuna (km 54), Kigoma – Kidahwe (km 36), Bagamoyo – Msata (km 64), Mwandiga – Manyovu (km 58), Ndundu – Somanga (km 60) na Chalinze – Segera – Tanga (km 242). Aidha miradi ambayo mchakato wa kuwapata Makandarasi wa kutekeleza ujenzi unaendelea ni Itigi – Tabora (sehemu ya Tabora - Nyahua (km 80), Sumbawanga – Mpanda, sehemu ya Sumbawanga – Chala (km 60), Singida – Babati – Minjingu (km 223), Tanga - Horohoro (km 65), Songea – Namtumbo (km 70), Tunduma – Sumbawanga (km 231) na Songea – Mbinga (km 100).

Barabara za Mikoa

Mwezi Disemba, 2005, Tanzania ilikuwa na mtandao wa Barabara za Mikoa wenye urefu wa jumla ya kilometa 18,957.4. Kati ya hizo, kilometa 330.4 zilikuwa za lami na kilometa 18,627 za changarawe. Hadi kufikia Disemba, 2008 mtandao wa Barabara za Mikoa ulikuwa na urefu wa jumla ya kilometa 19,246. Kati ya hizo, kilometa 635 ni za lami na kilometa 18,611 ni za changarawe. Vilevile, madaraja 45 yalijengwa na jumla ya madaraja 1,878 yalifanyiwa matengenezo.

No comments:

Post a Comment

My Headlines